VIVUTIO VYETU VYA UTALII; MAMLAKA YA HIFADHI YA NGORONGORO

Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro. 

Ikumbukwe na Ieleweke  hapa ya  kwamba  Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro si  eneo  ambalo  ni hifadhi ya Taifa  na vile  vile eneo  hili  la ngorongoro halipo chini  ya Shirika  la hifadhi za Taifa (TANAPA) na  badala  yake  ni Shirika  huru kama  jinsi  ilivyo  TANAPA likijitegemea. Kazi na majukumu ya TANAPA  na NGORONGORO zinafanana  katika  kuhifadhi  viumbe  hai na  makazi  yake  kuwa endelevu  kwa ajili  ya vizazi  vilivyopo na vijavyo. Lakini kwa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ni  eneo  ambalo ni hifadhi mseto ambapo  kuna viumbe hai  aina tatu  vikiishi  kwa  pamoja  ambavyo  ni watu ambao  zaidi ni  jamii ya Kabila   la Wamaasai,  mifugo yao  kama vile Kondoo,  Mbuzi na Ngombe na  tatu  ni Wanyamapori. 
HISTORIA YAKE:
Sababu  ya msingi iliyopelekea  kuanzishwa kwa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro  ni ukweli  wa mambo  ya  kwamba  jamii ya Kabila la Maasai  ilikuwa  ikiishi  katika maeneo  yote  ya Serengeti  na Ngorongoro kwa miaka  miangi   pamoja na  na Wanyamapori. Wamaasai  ni jamii  ya nilotiki  ambao  asili yao  ni  Kusini  mwa Sudani  na ni  jamii ya wafugaji  kiasili. Kwa kuwa jamii ya Wamaasai ilikuwa  ikiishi  ndani ya maeneo haya ya  uhifadhi  pasipo utaratibu maalumu na  mwongozo, jamii hii ya kabila la Wamaasai ilikuwa  katika janga  kubwa la wanyama  pori  kama vile  magonjwa  ya maambukizo ya wanyamapori  na majanga  mengineyo.
Hivyo  basi  serikali ya Wakoloni  Waingereza wakati wa kipindi  hicho  iliamua  kuanzisha  maeneo  mawili  tofauti  ya  uhifadhi. Eneo  moja la uhifadhi  litumike maalumu kwa ajili ya uhifadhi  wa wanyamapori pekee  ambayo  ndio  Serengeti  ya leo hii  na vile  vile  eneo jingine  la uhifadhi litumike  kama hifadhi  mseto  ambapo wamaasai wenyewe,  mifugo yao  pamoja na wanyamapori  wakiishi  kwa pamoja  yaani  (conservation). Hatimaye  Wamaasai  wote  waliokuwa  wakiishi Serengeti  ya  wakati wa kipindi  kile wakahamishiwa Mamlaka ya hifadhi  ya Ngorongoro ya leo hii.  Vile vile  malengo mengineyo yalikuwa  ni katika kulinda maslahi  ya jamii  ya kabila la Wamaasai  ambao  wameiishi  na Wanyamapori  pasipo  uharibifu  wowote  ule  kwa miaka  mingi. Jamii  ya kabila  la wamasai  wanachukuliwa  kuwa  ni  wahifadhi  asilia  kwa sababu  ya kuishi  na wanyamapori  kwa muda  mrefu  kihistoria.
Ikumbukwe   na ieleweke hapa  ya  kwamba  hifadhi  za Taifa  zote  zilizopo chini  ya Shirika la hifadhi za Taifa (TANAPA) pamoja  na mamlaka ya hifadhi  ya ngorongoro uanzishwaji wake ulikuwa ni  mwaka 1959. Kijiografia, mamlaka ya hifadhi ya ngorongoro inapatikana Mkoani Arusha.
MAANDALIZI YA USAFIRI:
Mahitaji ya fedha katika  safari  yenu  ya  matembezi  hifadhini  mamlaka  ya Ngorongoro.
KUANZISHWA  KWAKE:
Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro  ilianzishwa  mnamo mwaka 1959. Hii ilitokana  na  kumegwa  na kutengwa  eneo  lake  kutoka  Serengeti  na  kulifanya  eneo hili  kuwa ndio hifadhi mseto  pekee  Tanzania (Conservation) ambapo  watu, Wanyamapori na  mifugo  yao wakiishi  kwa  pamoja. Sehemu kubwa ya wananchi wanaoishi  ngorongoro  ni jamii ya kabila la wamaasai.

ENEO LAKE:
Ina ukubwa wa eneo  lenye  kilomita  za mraba  8300 (ambapo  ni sawa na maili za mraba  3200). Katika  ukubwa wa jumla  wa eneo  lote,  Bonde la ngorongoro (Ngorongoro Crater) ina ukubwa wa kilomita  za Mraba  zaidi ya  260 au asilimia 3,  Msitu wa asili  wa nyanda  za juu Kaskazini  asilimia  20,maeneo mengineyo ya milima asilimia 27,na maeneo ya tambarare ni asilimia 50.
UFIKAJI  HIFADHINI: 
Inafikika  umbali  wa kilomita 145 kwa njia ya  barabara  kutoka   hifadhi ya  Taifa  ya Serengeti,kilomita 60 kutoka hifadhi ya taifa ya  ziwa  Manyara, na  Kilomita  180 (maili  112) kutoka  Mkoani  Arusha. Ni mwendo wa saa  2 mpaka  3  kutoka Arusha. Saa 1  kutoka  hifadhi ya  ziwa Manyara  na saa 2 mpaka  3  kutoka Serengeti. Hii ni  hifadhi  ambayo  ipo katikati  baina ya ziwa  Victoria,  ziwa  kubwa  kuliko  yote  barani  Afrika, na mlima Kilimanjaro, Mlima mrefu kuliko yote  Afrika. 
MAUMBILE  ASILIA YA KIJIOGRAFIA  HIFADHINI:
Uwanda mpana  wenye  tambarare ,  milima, Milima yenye  Volkano, na  misitu  yenye  mandhari  nzuri  ya kupendeza.
HALI YA HEWA  USAWA WA BAHARI  HIFADHINI: 
Inaanzia  mita 1500 mpaka  3600 kutoka  usawa wa bahari. 
VIVUTIO VIKUU VYA UTALII  HIFADHINI:
Bonde la Ngorongoro (Ngorongoro crater),  Bonde la Empakai, Mlima  Oldoinyolengai, mlima  pekee  Tanzania  ambao  Volkano  yake  bado ni  hai.  Bonde  la Oldupai, sehemu  ambayo  ndio  chimbuko  la historia  yetu. Vile vile misitu yenye  mandhari  nzuri  yenye  kupendeza.
WANYAMAPORI WAPATIKANAO  HIFADHINI
Simba, Fisi, Nyumbu, Viboko, Swala Granti, Swala Tomi, Kongoni aina ya  Cokei,  Ngiri Wanyamapori, Pofu, Pundamilia, Duma, Mbogo (Nyati), Tembo Madume (Bonde la ngorongoro), Tembo majike na watoto nje ya bonde la  Ngorongoro. Viumbe hai ndege  ni pamoja  na mbuni, Tandawala,  Kanga na  wengineo wengi. Vile vile ndio  sehemu  pekee zaidi Tanzania kuwaona wanyamapori  aina ya faru zaidi katika bonde la Ngorongoro. 

MAMBO YA KUCHUKUA:
Vifaa vyote muhimu vinavyohusiana na safari yenu ya matembezi hifadhini; 
HUDUMA ZA  MAHITAJI  MENGINEYO:
Mambo ya ziada ya mahitaji yanayojitokeza na upatikanaji wake katika sehemu husika.   
UOTO WA ASILI  HIFADHINI:
Uoto wa asili katika mamlaka ya hifadhi ya  ngorongoro  inaangukia katika  uoto wa asili  wa milimani (Afro – Montane  region) na uoto mwingineo  tofauti  tofauti kama vile  tambarare zenye  nyasi  fupi  (short  grassy  plains) 
WAKATI WA KUTEMBELEA  HIFADHINI:
Mwezi wa Desemba mpaka  Februari.  Vile vile  mwezi  Mei  mpaka Julai.
HUDUMA ZA CHAKULA:
Je  mtakuwa  na mpishi  wenu?  Au mtajibebea  vyakula vyenu wenyewe?  Kama ndivyo sivyo, Je huduma za chakula  mtazipata wapi? 
Mamlaka  ya hifadhi  ya ngorongoro ipo  karibu sana na mji  wa Karatu  kwa upande  wa Kusini  ambapo  sehemu  nyingi hupatikana  zitoazo  huduma za vyakula.
HUDUMA ZA MALAZI AU KULALA:
Safari  yenu  ya  matembezi hifadhini ni lazima  izingatie  kama  mtalala ndani  ya hifadhi  (kupiga  kambi  au  mahema). Kama  hamtalala ndani  ya hifadhi, Je ni  mpangilio na utartibu upi mtakaouandaa?  Hii ndio  dira  itakayowapatia  picha  halisi ya mambo kama ni  kubeba  vifaa  vya kupigia  kambi  au  hapana. Kwa upande  mwingine,  nyumba za kulala wageni  katika mji wa Karatu zinapatikana.
GHARAMA ZA USAFIRI  WOTE:
Hii ndio dira elekezi itakayotoa picha halisi ya safari yenu ya matembezi hifadhini.  Haya  yote  ni baada ya kukamilisha  mambo  kama vile  maandalizi  ya usafiri, huduma  za chakula, malazi au  kulala  na mengineyo yatakayojitokeza kama vile   dharura.
MAMBO YA KUFAHAMU
Kama mtatumia usafiri maalumu  wa mamlaka ya  hifadhi  ya ngorongoro kuteremkia katika bonde la ngorongoro  basi kuna  ulazima  wa kuwepo  mawasiliano  kuweza kufahamu  kama  huduma  hiyo  ipo au haipo.Kama huduma hiyo haipo basi  utaratibu  mwingine  uandaliwe. Kufahamu haya  yote  ni lazima  kuwasiliana  na mamlaka  ya  hifadhi  ya  ngorongoro  kama  kuna  uwezekano  huo  upo. Je  ni Kampuni  zipi  nyinginezo mtakazozitumia  zinazotoa  huduma  hiyo  hifadhini?
MAMBO YA KUFANYA:
Watanzania watalii wa ndani ni vizuri wakaelimishana wao wenyewe
katika vikundi  vyao  kuhusiana na elimu  ya  huduma ya kwanza.
MAWASILIANO
Mamlaka ya hifadhi  ya Ngorongoro
S.L.P. 1, Ngorongoro
Simu;  +255 27 253 7006
+255 27 253 7019
+255 27 253 7007
Nukushi;
+ 255 27 253 7007
Tovuti;  www. Ngorongoro – Crater – africa.org.
Barua pepe; ncaa-info@africaonline.co.tz
ncaa-info@cybernet.co.tz
ncaafarm@cybertnet.co.tz)
MAMBO YA KUZINGATIA  HIFADHINI:
Kanuni na taratibu  za hifadhi  ni  muhimu  sana kutekelezwa ili  kuepuka  matatizo  ambayo  yanayoweza kujitokeza.


Ukweli kuhusu Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro. 
Ikumbukwe na Ieleweke  hapa ya  kwamba  Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro si  eneo  ambalo  ni hifadhi ya Taifa  na vile  vile eneo  hili  la ngorongoro halipo chini  ya Shirika  la hifadhi za Taifa (TANAPA) na  badala  yake  ni Shirika  huru kama  jinsi  ilivyo  TANAPA likijitegemea. Kazi na majukumu ya TANAPA  na NGORONGORO zinafanana  katika  kuhifadhi  viumbe  hai na  makazi  yake  kuwa endelevu  kwa ajili  ya vizazi  vilivyopo na vijavyo. Lakini kwa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ni  eneo  ambalo ni hifadhi mseto ambapo  kuna viumbe hai  aina tatu  vikiishi  kwa  pamoja  ambavyo  ni watu ambao  zaidi ni  jamii ya Kabila   la Wamaasai,  mifugo yao  kama vile Kondoo,  Mbuzi na Ngombe na  tatu  ni Wanyamapori. - See more at: http://tazamaramanitanzania.com/Mamlaka%20ya%20Hifadhi%20Ngorongoro.html#.U32gPii57gk


0 comments:

Post a Comment