MAELEZO YA MHE. LAZARO S. NYALANDU (MB), WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, KATIKA HAFLA YA KUMPONGEZA MHE. ZAKHIA H. MEGHJI, ) KWA KUTUNUKIWA UTUMISHI ULIOTUKUKA KATIKA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII: BANDA LA SABASABA LA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII,

Bibi Maimuna Tarishi; Katibu Mkuu – Wizara ya Maliasili na Utalii;
Bw. Selestine Gesimba; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,
Mhe. Zakhia Hamdani Meghji (Mb);Mgeni wetu Rasmi
Viongozi wa Wizara;
Watumishi;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana
Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kuungana na Watumishi pamoja na Wadau wa Wizara ya Maliasili na Utalii kukukaribisha tena katika Wizara yako ya Maliasili na Utalii. Aidha, napenda kuwapongeza Watumishi pamoja na Wadau wetu kwa Ushindi wa Banda tulioupata. Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii limekuwa Banda bora katika eneo la Wizara na Taasisi za Serikali. Natumaini kwa njia moja au nyingine, kwa kupitia ushindi huu tunaendelea kumuenzi Mama yetu Mhe. Zakhia Meghji kwa kazi nzuri aliyoifanya katika Wizara hii katika kipindi chake cha uongozi cha muda wa miaka tisa. Hivyo, Mhe. Meghji, tunapenda ushindi huu uwe zawadi mojawapo kwako leo hii.
Aidha, Mhe. Zakia Meghji, kama Katibu Mkuu alivyosema hapo awali, napenda kuchukua fursa hii kukupongeza kwa Nishani ya kipekee uliyotunukiwa na Mhe. Rais kwa kuitumikia vema Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mabibi na Mabwana,
Kwa kifupi Mhe. Zakhia Meghji ni Waziri pekee wa Wizara ya Maliasili na Utalii aliyeitumikia Wizara hii kwa muda mrefu zaidi kwa muda wa miaka tisa, na kwa mafanikio makubwa.
Mhe. Meghji,
Katika kipindi chote cha utumishi wako katika Wizara yetu, umeshiriki kikamilifu, kwa nguvu na moyo wako wote kuhakikisha kuwa Wizara hii inasimama imara na kutekeleza majukumu yake ya kutumikia umma wa Watanzania kwa ufanisi mkubwa. Napenda kubainisha baadhi ya mafanikio yaliyojitokeza wazi kutokana na uongozi wako katika sekta zinazosimamiwa na Wizara hii.
Sekta ya Utalii
(a) Katika kipindi cha unongozi wako Mhe. Meghji ulifanikisha kuundwa na kuzinduliwa kwa sera ya kwanza ya utalii ya mwaka 1999, ikizingatia mabadiliko mbalimbali yaliyokuwa yanaikumba dunia ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa karibu wa sekta binafsi katika. Aidha, ulizindua Mpango Kamambe wa Maendeleo ya Utalii wa mwaka 2002 (Tourism Master Plan). Miongozo hii ya utalii ndiyo misingi imara ya kuendeleza sekta ya utalii hapa nchini.
(b) Katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wako idadi ya watalii wanaoingia nchini iliongezeka kwa kasi kuliko katika kipindi chochote kingine. Idadi iliongezeka kwa asilimia 10 mwaka 1998 hadi kufikia ongezeko la asilimia 30 mwaka 1999; na idadi iliendelea kuimarika katika kipindi cha uongozi wako.
(c) Ushirikiano wako na Wizara nyingine za Serikali uliwezesha kujengwa barabara za kuwezesha utalii zikiwemo barabara ya Makuyuni-Ngorongoro kwa msaada wa Serikali ya Japani na barabara ziendazo katika hoteli zilizopo katika fukwe za Dar es Salaam. Mafanikio haya yalikuwa chachu ya kuongeza idadi ya watalii pamoja na mapato kutokana na sekta ya utalii.
(d) Ulifufua uanachama wa Tanzania katika Chama cha Wasafiri wa Utalii Afrika (African Travel Association) chenye makao makuu yake New York, nchini Marekani. Aidha, Ulikuwa Rais wa chama hicho kwa kipindi cha miaka saba na kufanikisha masuala kadhaa ya chama hicho. Fursa ya kuwa Rais wa ATA ilisaidia kuitangaza nchi yetu katika nyanja za utalii hususan katika soko la Marekani.
(e) Ulifanikiwa kuishawishi Serikali ya Ufaransa kutoa ufadhili wa ujenzi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Kampasi ya Bustani, ambacho matunda yake tunayaona kwa sasa kwa kuongezeka idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa katika tasnia ya ukarimu na utalii.
(f) Jengo hili la Maonyesho katika viwanja vya SabaSaba ni matokeo ya juhudi za uongozi wako.
Sekta ya Misitu na Ufugaji Nyuki
a) Ulisimamia mchakato na kuidhinishwa kwa Sera ya Taifa ya Ufugaji Nyuki (April, 1998) na Sera ya Taifa ya Misitu (April, 1998); Sheria ya Misitu na Sheria ya Ufugaji Nyuki (2002) na Programu za Taifa za Misitu na Ufugaji Nyuki (2001 – 2010). Sera na Sheria zote ni za kwanza kwa Tanzania huru. Hongera sana.
b) Kutokana na kuwa na Sera ya Taifa ya Ufugaji Nyuki (April, 1998), kuliifanya Tanzania kuwa ndio nchi pekee barani Afrika yenye Sera ya Ufugaji Nyuki. Sera iliweka msingi wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki na kuitangaza asali ya Tanzania katika soko la kimataifa.
c) Kutokana na kuwa na Sera ya Taifa ya Misitu (April, 1998) kuliwezesha yafuatayo:
i. Kuhimiza ushirikishwaji wa jamii katika usimamizi wa misitu. Hadi sasa Tanzania kuna misitu ya hifadhi kwa mpango wa ushirikishwaji takriban Hekta milioni 5.2. Aidha, mitandao ya jamii ya usimamizi wa misitu imeanzishwa na kuendelezwa.
ii. Kuanzishwa kwa mifuko ya uhifadhi wa rasilimali za misitu ambapo mifuko miwili ya uhifadhi wa misitu imeanzishwa ikiwemo (i) Mfuko wa uhifadhi wa misitu ya milima ya tao la mashariki yenye umihimu wa pekee katika uhifadhi wa bioanuai adimu na inayopatika nchini Tanzania pekee. Milima ya tao la mashariki ni moja ya “biodiversity Hot spots” duniani. (ii) Mfuko wa Misitu Tanzania – unaoangalia maeneo yote ya kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa ya kijani na mazingira salama.
iii. Kuanzishwa Wakala za usimamizi endelevu wa misitu; Kwa sasa kuna Wakala mbili za masuala ya misitu ambazo zimeanzishwa. Wakala hizo ni (i) Wakala wa mbegu za miti (TTSA) ili kuwa na mbegu bora za kuendeleza misitu; na (ii) Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kwa ajili ya usimamizi madhubuti na endelevu wa misitu.
d) Ulisimamia mchakato na uzinduzi wa kuanzishwa kwa Hifadhi Asilia ya Amani (Amani Nature Reserve) ambayo ni ya kwanza kwa Tanzania (1999).
e) Miradi mikubwa ni pamoja na mradi wa Benki ya Dunia (1998 – 2002) uliowezesha mchakato wa kuundwa kwa TFS na kupata Jengo la Mpingo ambalo ndio makao makuu ya Wizara kwa sasa.
f) Kutokana na usimamizi wako, Tanzania ilipata Nishani ya Equator (Equator Initiative Prize) kutokana na uhifadhi na usimamizi mahiri wa uoto wa asili (NGITILI) katika mkoa wa Shinyanga.
g) Mradi wa uendelezaji Ufugaji Nyuki uliwezesha kuongeza idadi ya wafugaji na hivyo kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao ya nyuki, na kukua kwa soko la asali ya Tanzania katika bara la Ulaya, Amerika, Asia na Afrika.
Sekta ya Mambo ya Kale
Katika kipindi cha uongozi wako shupavu, Sekta ya Malikale ilifanikisha kutekeleza mambo yafuatayo:
(i) Kuiwezesha Idara ya Mambo ya Kale kuhamia katika Wizara ya Maliasili na Utalii na kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya sekta hiyo pamoja na utalii;
(ii) Kuanzisha mchakato wa kuandaa Sera ya Malikale mwaka 2002 ambayo ilikamilishwa mwaka mwaka 2008 kwa lugha ya Kiswahili na kutafsiriwa katika lugha ya Kiingereza. Sera hii imesaidia kutoa mwelekeo na kupanua wigo wa uendelezaji wa malikale nchini kwa kugawa majukumu kwa wadau wa malikale;
(iii) Kubainisha Njia ya Kati ya Biashara ya Watumwa na Vipusa yenye urefu wa kilomita 1200 kutoka Ujiji, Kigoma mpaka Bagamoyo, Pwani; Aidha, ulianzisha mchakato wa Wizara ya Maliasili na Utalii kukubidhiwa kituo cha Makumbusho ya Dkt. Livingstone kutoka Halmashauri ya Mji wa Kigoma ambapo kilikabidhiwa rasmi kwa mwezi Aprili, 2006;
ii) Kukamilisha ujenzi wa Vituo vitatu vya kumbukumbu na taarifa katika maeneo matatu ya malikale - Michoro ya Miambani Kolo, Kondoa; Caravan Serai, Bagamoyo; na Isimila, Iringa mwaka 2005. Vituo hivi vinatumika katika kutoa taarifa kwa wageni kuhusu maeneo ya malikale nchini;
iii) Kuingiza eneo la Michoro ya Miambani, Kondoa katika orodha ya Urithi wa Taifa kwa kusaini Tangazo la Serikali (GN) mwaka 2004; na hatimaye kuingizwa katika orodha hiyo mwaka 2006. Kutokana na eneo hili kuwa katika orodha ya urithi wa dunia linapata misaada ya kiufundi kutoka taasisi za Kimataifa;
iv) Kushirikiana na wadau katika kukarabati na kuhuisha matumizi ya majengo ya Kihistoria kama vile Jengo la Ikulu, Hospitali ya Ocean Road, Kanisa la KKKT Azania Front na Kanisa la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam; Boma la Mikindani, Mtwara. Majengo haya yamekuwa mfano mzuri kwa wadau wa malikale kuhusu matumizi endelevu ya majengo ya kihistoria.
v) Kuwezesha kuanzishwa kwa kozi ya uhifadhi, usimamizi wa malikale na uongozaji wageni katika ngazi ya Cheti, Stashahada na Shahada katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2005. Kuanzishwa kwa kozi hizi kumewezesha kuwepo watalaam wa malikale katika soko la ajira nchini.
vi) Kudumisha ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa kuhusu uhifadhi, utunzaji na matumizi endelevu ya malikale. Baadhi ya ushirikiano huo ni Jumuiya ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kusini mwa Afrika; Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO); Baraza la kimataifa la Maeneo na Majengo ya Kihistoria (ICOMOS); na Baraza la Kimataifa la Makumbusho (ICOM);
vii) Kuwezesha Tanzania kujiunga na Kituo cha Kimataifa cha Mafunzo ya Uhifadhi na Ukarabati wa Mali za Utamaduni (ICCROM) mwaka 2004. Kupitia Shirika hili, watumishi wa Idara ya Mambo wanapata mafunzo ya uhifadhi na ukarabati wa maeneo ya malikale.
viii) Ulifanikiwa kuishawishi Serikali ya Sweden kutoa ufadhili wa Mradi wa Kujenga Uwezo wa Idara mwaka 2004. Kupitia Mradi huu, Idara imeweza kujenga uwezo wa watumishi wa idara ya Mambo ya Kale kitaaluma kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali na kupata msaada wa kiufundi kama vile vitendea kazi kama vile Kompyuta na vifaa vya usafiri;
Sekta ya Wanyamapori
Mambo muhimu uliyofanya wakati wa uongozi wako katika Idara ya Wanyamapori ni pamoja na;
o Uanzishaji wa Kamati ya Kugawa Vitalu (Block Allocation Advisory Committe);
o Kanuni za Uwindaji wa Kitalii za mwaka 2000;
o Kuanzisha Kanuni za WMAs 2005;
o Kupanua wigo wa Retention Scheme kwenye Mapori ya Akiba ya Moyowosi, Kigosi, Ibanda Rumanyika, Burigi/Biharamulo na Kimisi;
o Idadi ya Tembo na Wanyamapori wengine iliongezeka baada ya kufanya yafuatayo:
- Kuwapa motisha watumishi kwa kuboresha mazingira ya watumishi kama nyumba, ofisi na vitendea kazi vingine, na
- Kudhibiti ujangili,
o Idara kuongeza mapato kwa kiasi kikubwa;
o Kuanzisha na kutekeleza kwa mafanikio makubwa huduma kwa mteja (Client Service Charter);
o Kuanzisha mchakato wa kununua ndege mbili za Sekta ya Wanyamapori aina ya Caravan;
o Kuanzisha mchakato wa kupitia Sheria ya Wanyamapori (Wildlife Conservation Act. No.5 of 2009); na
o Kuweka saini Mkataba wa Ramsar (Ramsar Convention) 2000.
Ni kutokana na mafanikio niliyobainisha hapo juu, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliona inastahili kukutunuku nishani ya utumishi uliotukuka katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Muungano wetu. Nami napenda kuungana na Mhe. Rais kukupongeza kwa nishani hiyo.
Mhe. Meghji, ikiwa ni ishara ya kukupongeza kwa kutunukiwa nishani hiyo, kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii tunapenda kukupa zawadi zifuatazo.
1. Picha kutoka kwa Wadau
2. Taswira ya mnyamapori na
3. Ndoo ya asali
Asante sana


0 comments:

Post a Comment