JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII - TAARIFA KWA UMMA

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KINARA UANDAAJI BORA WA TAARIFA ZA KIFEDHA MWAKA 2013/2014

Wizara ya Maliasili na Utalii imetunukiwa tuzo baada ya kuwa mshindi wa kwanza kwa uandaaji bora wa taarifa za fedha (Financial Statements) kwa mwaka 2013/2014 kati ya Wizara, Idara. Wakala na Taasisi za Serikali. Tuzo hiyo imetokana na Wizara hiyo kukidhi vigezo vilivyoweka na Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu nchini (NBAA ambayo huandaa mashindano la uwekaji wa taarifa za kifedha kwa taasisi mbalimbali za hapa nchini kila mwaka. Mashindano hayo yalijumuisha washiriki 40 ambao waligawanywa katika makundi 11 kulingana na huduma wanazotoa.

Tuzo hiyo ilikabaidhiwa na Naibu Waziri wa fedha, Mhe. Adam Malima kwa Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Layson Mwanjisi aliyemwakilisha Katibu Mkuu kwenye hafla iliyofanyika Disemba 6, 2014 Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha. Bwana Mwanjisi aliikabidhi tuzo hiyo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Adelhem Meru ofisini kwake Mpingo house Disemba 11, 2014.

Akipokea tuzo hiyo, Dkt Meru alisema, ‘ushindi huu ni uthibitisho tosha kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii ipo makini katika masuala ya usimamizi wa fedha za umma.’ Aidha, Dkt. Meru aliwaasa watumishi kufanya kazi kwa bidii ili kuendelea kuwa vinara katika usimamizi wa rasilimali za Taifa.

Mbali na tuzo hiyo, Bw. Mwanjisi ametunukiwa cheti kwa kuwa mwasilishaji wa mada nyingi za jinsi ya kuwasilisha taarifa za kifedha kwa mfumo wa Kimataifa. Bwana Mwanjisi aliwasilisha jumla ya mada tano. Wizara inampongeza Bw. Layson Mwanjisi kwa tunzo hiyo ya cheti na kuwa kiongozi wa mfano katika Wizara ya Maliasili na Utalii.

NBAA huandaa mashindano hayo kila mwaka ambapo mashirika binafsi, taasisi na idara za serikali, hushindanishwa katika uandaaji wa taarifa za kifedha.

Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano


0 comments:

Post a Comment