RISALA YA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII MHE. LAZARO SAMUEL NYALANDU (Mb.) KUADHIMISHA SIKU YA TAIFA YA KUPANDA MITI TAREHE 1 APRILI 2015

Ndugu wananchi,
Leo, tarehe mosi Aprili ni Siku ya Taifa ya Kupanda Miti ambayo tunaiadhimisha kila mwaka.
Chimbuko la Siku ya Taifa ya Kupanda Miti ilikuwa ishara ya kuikaribisha Milenia mpya ambapo Serikali iliwahamasisha wananchi kupanda miti milioni mia moja mwanzoni mwa mwaka 2000.
Tangu mwaka 2004 maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Kupanda Miti yalianza kuratibiwa katika ngazi za mikoa.
Kila mkoa ulipewa fursa ya kupanga siku yake ya kupanda miti kulingana na majira ya mvua. Kwa hiyo Aprili Mosi, ni Siku ya Taifa ya Kupanda Miti na huadhimishwa kila mwaka Kitaifa. Katika siku hii wananchi mikoani mwao wanahamasishwa kupanda miti kwa wingi.
Aidha, katika mikoa ambayo haipati mvua mwezi Aprili wananchi wake wanatakiwa kupanda miti michache kuashiria maadhimisho ya siku hii. Miti mingine ipandwe wakati muafaka kufuatana na majira ya mvua katika mkoa husika.
Ndugu Wananchi
Katika maadhimisho ya mwaka huu yanayoongozwa na kauli mbiu isemayo ’MISITU NI MALI, PANDA MITI, napenda kuwaasa wananchi wote kushiriki katika zoezi la kupanda miti kikamilifu. Aidha, ifahamike kuwa misitu ni mali kwani inasaidia katika kuhifadhi mazingira pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi.
Pamoja na kupanda miti kwa ajili ya matumizi ya nyumbani wananchi wanatakiwa kupanda miti kwa wingi kwa ajili ya biashara. Soko la mazao ya misitu hapa nchini ni kubwa. Kwa sasa mbao zinazozalishwa kutoka katika mashamba ya serikali, kama vile Sao hill, Meru, Rongai na Buhindi, hazitoshelezi mahitaji ya soko.
Kwa kuwa kuna soko la uhakika la mazao ya misitu, nachukua fursa hii kuwaasa wananchi kutenga maeneo yao kwa ajili ya kupanda miti kibishara.
Ndugu Wananchi,
Ni dhahiri kuwa mahitaji ya mazao ya misitu yameongezeka sana nchini na siyo kwa mbao pekee, bali ni pamoja na kuni na mkaa ambavyo ndiyo chanzo kikuu cha nishati kwa takriban asilimia 90 ya Watanzania. Inakadiriwa kuwa asilimia 90 ya nishati yote inayotumika hapa nchini inatokana na miti.
Tathmini ya Misitu inaonesha kuwa kuna upungufu wa takribani ujazo 19.5 milioni za rasilimali mbao katika miaka 15 ijayo. Upungufu. huu utaongezeka kwa kasi kama hatutakuwa na mikakati ya kupanda miti ili kukidhi mahitaji haya.
Hatuna budi kuongeza juhudi za kupanda miti na kuhifadhi uoto wa asili uliopo. Pamoja na hayo, tunahitaji miti katika kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, viwandani, kilimo na kufua umeme.
Ndugu wananchi,
Tunatakiwa kupanda miti kwa wingi na kutunza iliyopo hasa ile ya asili ili kuhakikisha maji ya kutosha yanapatikana kwa maisha yetu na kuwezesha uchumi wa nchi kukua na kuongeza ajira na kipato cha kaya.
Ndugu wananchi
Natoa wito kwa wananchi wote nchini kujitokeza kupanda miti katika maeneo mliyoyachagua mikoani mwenu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kupanda miti kitaifa.
Kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera ambapo ndipo yanapofanyika maadhimisho ya siku ya kupanda miti kitaifa, nawasihi mjitokeze kwa wingi kupanda miti ifikapo tarehe 1 Aprili 2015 eneo la Omukajunguti kijiji cha Bugorora, Kata ya Bugorora, Wilaya ya Misenye, Mkoani Kagera
Asanteni kwa kunisikiliza, Nawatakia maadhimisho mema.
MISITU NI MALI, PANDA MITI
L.S. NYALANDU
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII
(CHANZO; WIZARA YA MALIASILI NA UTALII)


0 comments:

Post a Comment