TANZANIA YALAANI TUKIO LA UGAIDI NCHINI KENYA

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imelaani vikali shambulio la kigaidi lilitokea katika Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya na kusababisha vifo vya wanafunzi zaidi ya 150 pamoja na majeruhi .
Akiongea jana jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili wa Wanasheria kutoka nchi 20 Duniani, Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhe.Lazaro Nyalandu alisema mauaji hayo ni pigo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na hasa kwa sekta ya Utalii .
Mkutano huo wa Wanasheria unalenga masuala ya usuluhishi pindi migongano inapotokea miongoni mwa wafanyabiashara.
Aidha, Mhe. Nyalandu alisema kupitia mkutano huo Wanasheria wataweza kupanga mpango mkakati wa kushirikiana na wafanyabiashara katika kutatua migongano itakayotokea kati yao.
‘’Nchi yeyote ili iweze kuendelea ni lazima ifuate na kuheshimu utawala wa sheria, Utalii ndio sekta iliyoongoza kwa kuliingizia taifa mapato kutokana na kuheshimu utawala wa Sheria’’ Mhe. Nyalandu alisema.
Aidha, alisema kuwa matukio ya Ugaidi yamekuwa yakipunguza kasi ya ukuaji wa sekta ya Utalii kwani watalii wengi wanaopanga kutembelea vivutio vya utalii husitisha safari zao kutokana na hofu ya kushambuliwa na magaidi.
‘’Lakini hadi hivi sasa hakuna athari yoyote iliyotokea kwenye sekta ya Utalii licha jirani zetu Kenya kushambuliwa hivi karibuni. Napenda kuwahakikishia Watalii kuwa Tanzania ni salama.’’ Alisema Mhe. Nyalandu.
Alitoa wito kwa kila mmoja kuwa makini katika suala zima la ulinzi na usalama pindi anapotokea mtu ambaye hawamuelewi ni vyema kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola.


0 comments:

Post a Comment