Waziri Nyalandu alizindua Mkakati wa Utekelezaji wa Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii “WMA’

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu alizindua Mkakati wa Utekelezaji wa Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii (WMA's) kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Naura Springs, Arusha,tarehe 2/7/2015. Mkutano huo ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka Wizara ya Maliasili, Wenyeviti wa Muungano wa Jumuiya za WMAs zilizoidhinishwa, Wawakilishi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya USAID,WWF,FZS,AWF, na WCS. Aidha, viongozi wa WMAs, wawakilishi wa sekta binafsi na Maafisa wanyamapori wa Wilaya pia walihudhuria.
Mhe. Waziri alitoa wito wa kuboresha WMAs nchini na kusisitiza ushirikiano wa karibu na wizara. Vilevile alisema hadi sasa Tanzania inajivunia kuwa na WMA 21 zenye ukubwa wa kilometa za mraba 36,237.7 zilizoidhinishwa na kutangazwa katika Gazeti la Serikali. Mhe. Waziri aliongeza kuwa WMA nyingine 17 ziko katika hatua mbalimbali za uanzishwaji.
Mhe. Waziri Nyalandu alipongeza waandaaji wa mkutano huo na kusema kuwa mkutano huu ni wa kwanza kufanyika na kukutanisha Wizara, Jumuiya zilizoidhinishwa pamoja na wawekezaji wa WMAs .
Mkutano huo ulilenga kubadilishana ujuzi na uzoefu wa utekelezaji wa shughuli za WMAs; kuwa na uelewa wa pamoja na namna bora ya utekelezaji wa shughuli za WMAs na kupata mwelekeo wa pamoja wa uendeshaji wa WMA’s


0 comments:

Post a Comment