SERIKALI YA TANZANIA KWA KUSHIRIKIANA NA UFARANSA KUENDELEZA MAPANGO YA AMBONI TANFA

SERIKALI kwa kushirikiana na washirika wake wa maendeleo nchini imekusidia kuliendeleza eneo la Mapango ya Amboni yalioko mkoani Tanga ikiwa ni hatua ya kuboresha maisha ya wanajamii wanaolizunguka eneo hilo.
Hayo yameelezwa mapema wiki hii na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu kwenye ziara ya pamoja mkoani Tanga na Balozi wa Ufaransa nchini, Bw. Marcel Escure.
Mhe. Waziri amesema serikali kwa kushirikiana na Ufaransa inaanza kuangalia mpango mkakati wa kuendeleza eneo la Mapango ya Amboni lenye ukubwa wa hekta takribani 40 kwa miaka mia moja ijayo.Amesema kuwa mpango huo utaendelea kuruhusu wananchi kuendelea kufanya shughuli mbalimbali wanazoendelea kuzifanya ndani ya mapango hayo kama vile kuabudu.
Mhe. Nyalandu aliongeza kuwa atatumia nafasi yake kuhakikisha anashirikiana na wadau wengine serikali ikiwa ni pamoja na serikali ya mkoa wa Tanga ili eneo la Mapango ya Amboni liwe mahususi kwa mambo ya elimu pamoja na kuwa eneo maalum la kuendeleza utalii unaohusiana na mambo ya kale.
Sambamba na hilo, Mhe. Nyalandu amesema katika mpango huo wataangalia uwezekano wa kuongeza baadhi ya wanyama marafiki ili watalii watakaofika eneo hilo waweze kujionea rasilimali zingine zilizopo nchini.
Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini, Bw. Marcel Escure amesema eneo la Amboni ni moja ya maajabu ya asili duniani yanayovutia na kuhitaji kutangazwa na kutunzwa ili kuongeza idadi ya watalii pamoja na wanasayansi mbalimbali duniani waweze kufikana kufanya tafiti zao.
Bw. Escure aliongeza kuwa, Serikali yake kama itatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha eneo la Mapango ya Amboni linakuwa moja kati ya vivutio vikubwa vya utalii nchini.
Hata hivyo, Balozi huyo aliitaka serikali kuangalia uwezekano wa kuliingiza eneo hilo katika Orodha ya Vivutio vilivyopo katika Urithi wa Dunia kutokana na mvuto asilia ililonalo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Mambo ya Kale, Bw. Donatus Kamamba amesema pamoja na changamoto kubwa ya rasilimali fedha na watu eneo hilo linatunzwa kikamilifu kutokana na umuhimu wake katika sekta ya elimu na utalii duniani.


0 comments:

Post a Comment