WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, MHE. LAZARO NYALANDU, ASEMA SUALA LA UHIFADHI WA WANYAMAPORI NI JUKUMU LA KILA MTU.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu, amesema kwamba suala la uhifadhi la Wanyamapori dhidi ya Ujangili ni kila mtu, hivyo Jumuiya za Kimataifa ni lazima ziungane kikamilifu na Tanzania kwa kuhakikisha kuwa Wanyamapori wanaendelea kuwepo kwa ajili manufaa na maendeleo endelevu ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

Amesema hayo leo jijini, Dar es Salaam , kwenye hafla fupi iliyofanyika katika stesheni ya TAZARA kabla ya kuanza kwa safari ya mabalozi wa China na Umoja wa Nchi za Ulaya kwenda kutembelea pori la akiba la Selous kwa usafiri wa treni ikiwa ni mwendelezo wa urafiki kati ya nchi hizo ulioasisiwa na Mwalimu Nyerere.
Hafla hiyo imehudhuriwa na balozi wa China nchini Tanzania, Dr. Lu Youqing, Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP) , Alvaro, Rodriguez, Mkurugenzi Mtendaji wa TAZARA, Bw. Ronald Phiri, Katibu Mkuu wa Wizara ya fedha, Bi,. Dorothy Mwanyika , wanafunzi na baadhi ya viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mhe. Nyalandu, amesema suala la uhifadhi wa wanyamapori ni jukumu la kila mtu bila kujali rangi wala taifa analotokea, hivyo ni lazima kila mmoja ahakikishe kwa gharama yoyote wanyamapori waliopo hatarini kutoweka kutokana na watu wachache wasio na uzalendo wanaojihusisha na ujangili wanakamatwa na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.

Mhe. Nyalandu, amesisitiza kuwa kasi ya kutokomeza ujangili katika pori la akiba la Selous imekuwa na mafanikio makubwa ambapo takribani miezi sita sasa hakuna tembo yoyote aliyeuawa.

‘’Najisikia fahari sana kwa ushirikiano mkubwa ninaoupata kutoka kwa Mhe. Rais Jakaya Kikwete katika kuhakikisha wanyamapori wanalindwa na kuhifadhiwa , kutokana na jitihada hizi hadi sasa katika pori la akiba la Selous hakuna mzoga wowote ulioripotiwa kuonekana katika pori hilo’’ Mhe. Nyalandu alisisitiza.

Pia alisema kwamba askari wanyamapori katika pori la akiba la Selous wamekuwa ni mfano wa kuigwa kwa kufanya kazi usiku na machana kwa kuhakikisha kuwa hakuna tembo yoyote anayeuawa na majangili katika eneo hilo.

‘’ Nachukua nafasi hii kuwatia moyo askari wanyamapori wote wanaojitolea maisha yao kwa ajili ya kuwalinda wanyamapori ’’ Mhe. Nyalandu alisema.

Mhe Nyalandu, ameipongeza Serikali ya Jamhuri wa Watu wa China kwa kushirikiana na Tanzania kama ni njia moja wapo ya kumuenzi Mwalimu Nyerere aliyeasisi, Kwa kufanya safari ya Mabalozi hao kwenda katika Pori la akiba la Selous na baadhi ya wanafunzi kwa nia kujionea na kujifunza juu ya umuhimu wa kuhifadhi wanyamapori.

Aidha, Mhe Nyalandu, ameahidi wanafunzi mia moja wa Kitanzania kwenda nchini China mwakani ikiwa ni mwendelezo wa urafiki wa nchi hizi mbili kwa lengo la kujifunza juu ya umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori.

Amesisitiza kuwa wanafunzi hao wataweza kuwa mabalozi wazuri wakuielezea Tanzania kwa kuwa na vivutio vya Utalii vya kipekee ambavyo havipatikani popote ulimwenguni isipokuwa Tanzania.

Naye Balozi wa China Dr. Lu Yuqing amesisitiza kwamba ataendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania kwenye masuala ya kiuchumi pamoja na kuhakikisha wanyamapori wanalindwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

Dr. Lu Yuqing ameahidi kutoa msaada kwa nchi ya Tanzania ya mabehewa kumi na nane ikiwa ni njia ya kuweza kuifanya TAZARA kujizatiti kuwahudumia watu wa Tanzania na Zambia katika suala la usafiri wa treni .

Mbali na hafla hiyo, pia kuliambatana na tendo la kusaini vitabu vya ushirikiano kati ya nchi mbili ikiwa ni ishara ya kuendeleza urafiki ambapo Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dorothy Mwanyika ameishukuru nchi ya China kwa kuwa mstari wa mbele kuisaidia Tanzania kimaendeleo katika Nyanja zote.


0 comments:

Post a Comment