MIZENGO PINDA MGENI RASMI SIKU YA KUMBUKUMBU YA KIFO CHA CHIFU MKWAWA

WAZIRI Mkuu Mizengo Kayanza Pinda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Chifu Mkwawa yatakayofanyika katika kijiji cha Kalenga, Iringa Vijijini Julai 19, mwaka huu.

Siku moja kabla ya kilele cha maadhimisho hayo (Julai 18), kutakuwepo na kongamano la wazi litakalofanyika katika Chuo Kikuu cha Mkwawa litakalo jadili mada mbalimbali zitakazolenga kumkumbuka Chifu Mkwawa na utalii.

Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na kamati yake ya utalii ya mkoa iliazimia kuwepo na maadhimisho hayo kama moja ya njia ya kumuenzi shujaa huyo na kukuza utalii mkoani hapa.

Kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo yatakayokuwa yakifanyika kila mwaka, yalikuwa yafanyike mwaka jana lakini yalishindwa kufanyika kwasababu ya ukosefu wa rasilimali fedha.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho hayo, John Kiteve alisema; “mwaka huu tunafanya maadhimisho haya baada ya wadau mbalimbali kujitokeza na kutuunga mkono.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (IUCO), Gibson Sanga ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya maandalizi alisema chuo chao kwa kupitia mradi wake wa Kuendeleza Utamaduni Nyanda za Juu Kusini kimechangia Sh Milioni 16 kufanikisha maadhimisho hayo.

“Tumetoa kiasi hicho cha fedha, tunajua ni kidogo lakini uzalendo ukitumika katika kufanikisha shughuli hii tutafanikiwa,” alisema.

Waliziomba halmashauri za mkoa wa Iringa kwa muhimu wa shughuli hiyo na nafasi walizonazo wachangia gharama zikiwemo zamavazi ya kijadi na kusafirisha wazee wa kimila hadi katika eneo la tukio.

Mkwawa au kwa jina refu Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga alizaliwa mwaka 1855 na kufariki Julai 19, 1898. Alikuwa shujaa wa kweli katika kuupinga ukoloni na historia yake imeendelea kuenziwa duniani kote.

Alikuwa chifu na kiongozi mkuu wa kabila la Wahehe; aliongoza vita dhidi ya upanuzi wa ukoloni wa Ujerumani mwishoni mwa karne ya 19 kabla hajajiuwa mwenyewe kuepuka kukamatwa na kuuawa na wakoloni hao.

Kwenye kikao cha wadau wa utalii kilichofanyika mjini Iringa hivi karibuni kwa uratibu wa Mradi wa Kuimarisha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Gerald Guninita alinukuliwa akisema “…wakati umefika sasa tuwe na kumbukumbu ya shujaa huyo itakayowafanya wana Iringa kukumbuka historia ya kiongozi wao.”

Alisema kwa kuwa mkoa wa Iringa unataka kuwa kitovu cha utalii kwa mikoa ya nyanda za juu kusini, kuendeleza vyanzo vyake vya utalii ni pamoja na kuhenzi ipasavyo historia ya Chifu Mkwawa.

“Zipo jitihada za kutafuta vivutio mbalimbali vya utalii katika mkoa wetu kwa lengo la kuvitangaza, wakati tukifanya hivyo ni muhimu pia tukaboresha na kuvitangaza sana vivutio vilivyopo,” alisema.


0 comments:

Post a Comment