WAZIRI NYALANDU AZINDUA KAMPENI MPYA DHIDI YA UJANGILI

Waziri wa Maliasili na Utalii , Mhe. Lazaro Nyalandu kwa kushirikiana na Asasi ya Kimataifa ya WildAid na African wildlife Foundation wamezindua kampeni mpya ya kuongeza ufahamu na kuelimisha jamii kuhusu tatizo la ujangili nchini.
Akizungumza jijini Dares Salaam, Mhe. Nyalandu alisema kuwa kampeni hiyo itaongeza mwamko kwa Taasisi za kiraia katika kulinda tembo na wanyama wengine.
Katika uzinduzi huo, ulihudhuriwa na viongozi wa dini zote nchini, Wadau wa Uhifadhi wa ndani na nje ya nchi pamoja na Balozi wa Marekani nchini Tanzania na Mwakilishi kutoka China.
Katika uzinduzi wa kampeni hiyo iitwayo ‘’ UJANGILI UNATUUMIZA SOTE’’ Mhe. Nyalandu alisema Kampeni hiyo ni hatua muhimu katika mapambano dhidi ya Ujangili na pia itatoa mwamko kwa wananchi wote nchini kushiriki katika mapambano ya dhidi ya Ujangili.

Alisema vita dhidi ya Ujangili ni yetu sote hivyo ni lazima Asasi za Kimataifa zishiriki kwani serikali ya Tanzania pekee ni vigumu kushinda vita hii, licha ya mafanikio makubwa yanayoonekana hivi sasa chini ya Serikali ya Mhe. Rais Kikwete katika vita hivyo.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania Bw. Mark Childress alisema hatua iliyochukuliwa na China ya kusitisha ununuzi wa bidhaa za tembo nchini mwake ni mafanikio makubwa katika kukomesha vita dhidi ya ujangili Barani Afrika hususani nchini Tanzania.
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa Watanzania kushiriki katika kuhamasisha na kukataa kujihusisha kutumiwa na watu wachache wenye uchu wa utajiri wa haraka haraka kwa kupitia biashara haramu ya meno ya tembo.
Kwa upande wa Mkurugezi Mtendaji wa WILDAID, Peter Knights alisema ‘ Kauli mbiu ya Kampeni hii “UJANGILI UNATUUMIZA SOTE “ inawakumbusha wale wote wanaojihusisha na Ujangili wa kuua tembo na kusafirisha meno ya tembo kwenda nje wanatuumiza wa Tanzania sote.
Dkt. Patrick Bergin, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wildlife Foundation, alisisitiza kuwa Ujangili unachafua jina la Tanzania nchi ambayo
ina sifa ya kuwa na hifadhi kubwa ya tembo.
Kwa upande wa viongozi wa dini, Shekhe Alhad Musa wa Dar es salaam alisema Ujangili ni dhambi hivyo wale wote wanaojihusisha ni chukizo mbele ya Mwenyezi Mungu.
Naye, Msanii Maarufu wa Kizazi kipya wa Bongo Fleva , Ali Kiba ambaye kwa sasa ni Balozi wa kupambana na Ujangili nchini amesema atatumia uwezo wake wote katika kuwamasisha Watanzania kushiriki katika mapambano dhidi ya Ujangili kwa kuwa baadhi ya tembo wadogo wamekuwa wakibaki yatima kwa kuwapoteza wazazi wao wote kwa kuuawa na majangili.


0 comments:

Post a Comment