HABARI KUTOKA BODI YA UTALII: BI DEVOTA MDACHI ATEULIWA MKURUGENZI MWENDESHAJI TTB

Bi Devota Mdachi
Na: Ripota wetu
Hatimaye Bodi ya Utalii Tanzania imepata Mkurugenzi Mwendeshaji baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua kuanzia tarehe 23 Oktoba, 2015 aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo Bibi Devota Mdachi kushikilia wadhifa huo wa juu kabisa katika Bodi hiyo.
Bi Devota Mdachi ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa Masoko wa TTB amekuwa akikaimu nafasi hiyo ya Mkurugenzi Mwendeshaji kwa miaka miwili kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mwendeshaji anakuwa mwanamke wa kwanza nchini kushikilia wadhifa huo katika Bodi ya Utalii toka ilipoanzishwa mwaka 1993.
Bi Devota Mdachi aliajiriwa na Bodi ya Utalii Tanzania kama Afisa Habari za Utalii katika tawi la Arusha mwaka 1994 kabla ya kuhamishiwa Dar es salaam mwaka 1998. Mwaka 2000 alipandishwa cheo na kuwa Afisa Habari za Utalii Mwandamizi na baadae Afisa Habari za Utalii Mkuu mwaka 2004 kabla ya kuteuliwa kuwa Afisa Masoko Mkuu mwaka 2010.
Mwaka 2011 Bi Mdachi alifanyakazi katika Idara ya Masoko na Mawasiliano ya Shirikisho la Utalii la nchi
za kusini mwa Afrika – RETOSA nchini Afrika Kusini
kwa muda miezi mitatu kabla ya kurejea mwaka June, 2011 na kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Masoko mwaka 2014.
Mdachi ambaye pia ni miongoni mwa wanawake watano wa Tanzania walioshinda tuzo ya wanawake ya Mwl Nyerere (Mwl Nyerere Golden Award Women Achievers) ya mwaka 2015, ana shahada ya kwanza ya Uhusiano wa Kimataifa na lugha ya Kifaransa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Aidha ana shahada ya Uzamili katika Utalii Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Post graduate certificate ya Utalii kutoka shule ya Kimataifa ya Utalii iliyoko Rome Italia.


0 comments:

Post a Comment