Mwanasoka bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani ya Afrika Mbwana
Samata huenda akatunukiwa heshima ya kuwa balozi wa heshima wa Tanzania
endapo mazungumzo yanayoendelea baina ya TTB na mawakala wa mchezaji
huyo yatazaa matunda.
Bodi ya Utalii Tanzania imedhamiria kumtumia mchezaji huyo katika
kuitangaza Tanzania kama eneo la utalii pamoja na vivutio vyake vya
Utalii duniani kwa lengo la kuvutia watalii zaidi nchini.
“Tumeanza mazungumzo na mawakala wa mchezaji huyo ingawa bado
hatujafikia muafaka, wenzetu upande wa pili wameomba tuwape muda zaidi
wakatafakari zaidi” alidokeza Bw. Geofrey Tengeneza. Alisema mawakala wa
Samata walikuja katika meza ya mazungumzo wakiwa na mtazamo wa
Kibiashara zaidi wakati sisi tunalenga katika mtazamo wa kutanguliza
uzalendo badala ya biashara.
Endapo pande hizo mbili zitaafikiana Mbwana Samata ataungana na mabalozi wengine wa heshima ambao
pamoja na mambo mengine husaidia kuutangaza utalii wa Tanzania.
Mabalozi hao na nchi zao katika mabano ni pamoja na Dkt Costa Tungaraza
(Australia), Bw. Patrick Steenburg (USA), Bw. Macon Dunnugan (USA), Dkt.
Philip Imler (USA) na Bibi Flavian Matata (USA).
Mbwana Samata ni mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania ambaye hivi
karibuni alifanikiwa kuwa mfungaji bora na mchezaji bora barani Afrka
kwa wachezaji wanao cheza ndani ya Afrika.
0 comments:
Post a Comment