PROF. MAGHEMBE AZINDUA KITABU CHA KUHAMASISHA ULINZI WA TEMBO NA FARU (TEMBO - FARU WANA HAKI YA KUISHI TANZANIA)

Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Mhe. Ally Hassan Mwinyi (kulia) akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kitabu cha kuhamasisha ulinzi wa Tembo na Faru pamoja na kupiga vita ujangili kilichoandikwa na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es Salaam jana katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwl. J.K. Nyerere, Dar es Salaam. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akionesha kitabu hicho kwa wajumbe walioshiriki hafla hiyo kama ishara ya kukizindua rasmi kwa niaba ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Mhe. Ally Hassan Mwinyi (kulia) akiteta jambo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akimkabidhi Mwanasiasa Mkongwe nchini ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa chama cha CUF, Prof. Ibrahim Lipumba nakala ya kitabu hicho. Wapili kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Salum.
Picha ya pamoja.

------------------------------------------------------------------

Rais Mstaafu wa Awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Ally Hassan Mwinyi ametoa wito kwa watanzania kuongeza juhudi katika kusaidiana na Serikali kupiga vita ujangili hapa nchini.


Wito huo umetolewa jana jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa kitabu cha “Tembo-Faru wana haki ya kuishi Tanzania” kilichoandaliwa na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar  es salaam na kuzinduliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe kwa niaba ya Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli.

Rais mstaafu huyo, amesema kumekuwa na tatizo la mauaji ya wanyamapori hapa nchini ambayo ni dhambi na ni kinyume na kusudio la Mungu kwa kuwa wanyama hao wana haki ya kuishi kama viumbe wengine.

“Kumekuwa na matukio mengi ya uuaji wa wanyamapori ikiwemo tembo na faru na hivyo kupunguza rasilimali ya taifa kwa vizazi vijavyo na pia kitendo hicho ni kinyume na kusudio la Mungu hivyo ni vizuri kuwatunza, kuwapenda, kuwaendeleza na kuwalinda wanyama hao kwani ni moja ya vivutio vinavyochangia pato la Taifa” aliongeza Rais Mstaafu  Mwinyi.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe amesema kuwa Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na mbuga nzuri na bora duniani baada ya nchi ya Brazil na kusisitiza ni muhimu kwa watanzania wote kutunza rasilimali za taifa ikiwemo mbuga za wanyama na wanyamapori.

Aliongeza kuwa wanyamapori ni muhimu sana katika maisha ya kila mtanzania kwa kuwa kupitia utalii wanachangia asilimia 17.5 ya pato la taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za nje (foreign currency) hivyo hakuna budi kwa kila mtanzania kupiga vita ujangili ambao.
Alisema kuwa jumuiya ya ujangili ni kubwa ambayo inahusisha  makundi mbalimbali ikiwemo watengenezaji wa silaha za kuua tembo, waagizaji wa meno ya tembo, wasambazaji na watu mashuhuri ambao wanatumia nyumba zao kuhifadhina kununua meno ya tembo.


Kitabu cha “Tembo-Faru wana haki ya kuishi Tanzania” kimetayarishwa na kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es salaam kikiwa na lengo la kuwaelimisha waanadamu juu ya umuhimu wa kutunza mazingira na viumbe vilivyopo kwa faida yao na vizazi vijavyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum alisema jumla ya vitabu 5,000 vimechapishwa kwa ufadhili wa shirika la kimataifa la WILDAID, Jumla ya nakala milioni 20 zinahitajika kuchapishwa katika lugha tofauti na kusambaza katika nchi mbalimbali duniani na hivyo kuwaomba wadau mbalimbali kuchangia gharama za uchapishaji huo ambao kwa kila kitabu kimoja kinagharimu dola kimarekani 12.

Akizungumzia uchangiaji huo, Waziri Maghembe alisema kuwa Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania (TWPF) utachangia milioni 20 kuwezesha uchapishaji wa vitabu hivyo na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kuunga mkono juhudi za vingozi wa dini na Serikali katika kulinda na kuhifadhi Malisili za taifa kwa kuchangia uchapishaji wa kitabu hicho na kulinda Malisili za taifa.


0 comments:

Post a Comment